Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inasema dunia iko mbioni kuUtokomeza ugonjwa wa UKIMWI ifikapo mwaka 2030 mara tu programu muhimu za afya zitakapofadhiliwa kikamilifu.
Asilimia 65 ya watu wanaoishi na VVU wanaishi katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara. Hata hivyo eneo hilo limepiga hatua kubwa katika kuutokomeza UKIMWI.
Kwa mujibu wa Shirika la kupambana na ugonjwa wa ukimwi la Umoja wa Mataifa UNAIDS, nchi za Botswana, Eswatini, Rwanda, Tanzania na Zimbabwe zimefikia lengo la ’95-95-95′.
Hii ina maana kwamba asilimia 95 ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU) wanajua hali yao ya VVU, na asilimia 95 ya wale wanaojua hali zao wanapokea matibabu ya kurefusha maisha. Asilimia 95 ya watu wanaopokea matibabu hufubaza virusi, hatua ambayo huondoa kabisa nafasi ya kusambaza virusi kwa wengine.
Nchi zingine 16 zinakaribia kufikia lengo hilo, zikiwemo 8 zaidi katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Kukomesha UKIMWI ni fursa kwa viongozi wa siku hizi kuwa mfano mzuri,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Winnie Banayima.
Alisema, “Inaokoa mamilioni ya maisha na kulinda afya ya kila mtu. Inaonyesha kile ambacho uongozi unaweza kufanya.”
Lakini UNAIDS imebainisha kuwa nchi za kipato cha chini na cha kati zina upungufu wa bajeti wa dola bilioni 8.5.
“Ukweli na takwimu za ripoti hii hazionyeshi kwamba tuko katika mwelekeo huo, lakini tunaweza kuwepo,” alisema Byanyima.
Lakini changamoto kadhaa zimesalia kutatuliwa. Kila wiki, maambukizi mapya 4,000 ya VVU huongezwa kwa vijana wa kike na wakiume.
Na licha ya maendeleo, asilimia 63 ya maambukizi mapya ya VVU mwaka 2022 yalitokea kwa wanawake na vijana katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Wasichana waliovunja ungo wako hatarini nchini Botswana, kusini mwa Afrika. Inajulikana kama ‘ngono kati ya vizazi’, ambapo wanaume wakubwa huwafuata wasichana wadogo.
Gaon ni mwanamke mwenye umri wa miaka 32 ambaye alipata VVU akiwa bado msichana wa shule.
“Kuna jamaa wa karibu alikuwa akinisaidia sana. Alikuwa na umri mara mbili yangu, katika miaka ya 30s. Nilimuamini. Alitumia fursa hiyo na kufanya ngono nami.”
Gaon amekuwa akitumia dawa za kurefusha maisha tangu 2012. Mama wa watoto wawili, alisema watoto wake hawana VVU. Sasa anafanya kazi kama mwanaharakati akipiga kampeni.
Kwa mujibu wake, hata sasa jamii haiko tayari kujadili kwa uwazi ‘ubakaji’ na ‘unyonyaji wa kingono’.
“Katika baadhi ya siku, mimi hupata taarifa kutoka kwa wanawake hadi watano, wengi wao wakiwa wakubwa kuliko mimi, ambao wameambukizwa VVU kutoka kwa jamaa. Tunaweza kufanya nini ikiwa wanaume hawasikii,” anahoji
Nguvu ya maombi
Takwimu zote zinaonyesha kuwa wanaume wanasitasita kutafuta huduma za afya kuliko wanawake walioambukizwa VVU.
Botswana inatumia viongozi wa kidini kujaribu kubadili mitazamo ya wanaume na kuzuia maambukizi ya VVU.
“Asilimia tisini na tano ya watu wanaoishi na VVU nchini Botswana wanajua hali zao. Wasiojua wengi wao ni wanaume,” alisema Machakaga Mpho Moruakgomo, kiongozi wa dini ya Kikristo na kundi la madhehebu mbalimbali linalokabiliana na tatizo hilo.
“Kwa sababu watu wanaheshimu viongozi wa kidini, tunatumia hiyo kuzungumza na wanaume kuhusu haja ya kupima na, ikiwa hali itathibitishwa, tunawaunganisha na matibabu.”
Alitaja viongozi wa Waislamu, Wahindu na Wabahai pia wanajihusisha na wakazi wa eneo hilo na kusema kwamba wanaenda siku hadi siku wakibeba ujumbe.
Kampeni hiyo inaitwa ‘Brothers Arise-Nanogang’ ambayo imechochewa na sehemu ya wimbo wa taifa wa nchi hiyo.
Mchungaji Moruakgomo wa kanisa hilo anasema, “Kuna ushirikina mwingi kuhusu VVU. Sisi viongozi wa dini pia tulihusika na hilo.”
Alitaja kuwa wamewalaumu walioambukizwa na kusema kwamba wanapaswa kukiri makosa yao na kuomba msamaha.
Ontiretse Lethare, mkuu wa Shirika la Kitaifa la Kukuza UKIMWI na Afya, alisema Botswana iko mbioni kutokomeza VVU ifikapo mwaka 2030. Anasema viongozi wa kidini wanaweza kuwa na jukumu muhimu kwa hilo.
Hali ikoje kwingineko duniani?
Katika sehemu zingine za ulimwengu, mwelekeo sio mzuri sana. Kulingana na Umoja wa Mataifa, robo ya maambukizo mapya ya VVU yalitokea katika eneo la Asia Pacific mnamo 2022.
Ulaya Mashariki na Asia ya Kati pia zinakabiliwa na maambukizo mapya kila wakati. Hali kama hiyo imeibuka katika Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.
Umoja wa Mataifa umetaja ukosefu wa huduma za kudhibiti VVU kwa watu waliotengwa na sheria ambazo zinahalalisha jamii ya mapenzi ya jinsia moja, LGBTQ+.
Lakini matibabu yanayoitwa PrEP yanatoa matumaini. Aambodia ya Asia Mashariki inatoa dawa hiyo bure kwa wafanyabiashara ya ngono walio hatarini na jamii ya wapenzi wa jinsia moja na waliobadili jinsia.
Kidonge cha kila siku hutumiwa kutibu VVU. Watu wasio na VVU wanaweza pia kuchukua kama dawa ya kuzuia.
#Nchi #tano #Afrika #zinakaribia #kuutokomeza #ugonjwa #UKIMWI #Ripoti #Fastestsmm #News #Swahili